Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 5:16-30 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Watu wengi walifika kutoka katika miji ya kandokando ya Yerusalemu, wakiwaleta wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa.

17. Kisha, kuhani mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo, wakawaonea mitume wivu.

18. Basi, wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu.

19. Lakini usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia,

20. “Nendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uhai huu.”

21. Mitume walitii, wakaingia hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha.Kuhani mkuu na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu na halmashauri yote ya wazee wa Wayahudi, halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume.

22. Lakini hao watumishi walipofika huko hawakuwakuta mle gerezani. Hivyo walirudi, wakatoa taarifa mkutanoni,

23. wakisema, “Tulikuta gereza limefungwa kila upande na walinzi wakilinda milango. Lakini tulipofungua hatukumkuta mtu yeyote ndani.”

24. Mkuu wa walinzi wa hekalu na makuhani wakuu waliposikia habari hiyo wakawa na wasiwasi, wasijue yaliyowapata.

25. Akafika mtu mmoja, akawaambia, “Wale watu mliowafunga gerezani, hivi sasa wamo hekaluni, wanawafundisha watu.”

26. Hapo mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na watu wake walikwenda hekaluni, akawaleta. Lakini hawakuwakamata kwa nguvu, maana waliogopa kwamba watu wangewapiga mawe.

27. Basi, wakawapeleka, wakawasimamisha mbele ya Baraza. Kuhani mkuu akawaambia,

28. “Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo cha mtu huyo.”

29. Hapo Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, “Lazima tumtii Mungu, na siyo binadamu.

30. Mungu wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya nyinyi kumuua kwa kumtundika msalabani.

Kusoma sura kamili Matendo 5