Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 28:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Wao wakamwambia, “Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako.

22. Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali.”

23. Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya ufalme wa Mungu, akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia sheria na maandiko ya manabii.

24. Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini.

25. Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili: “Kweli ni sawa yale Roho Mtakatifu aliyowaarifu wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya

26. akisema:‘Nenda kwa watu hawa ukawaambie:Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa;kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

27. Maana akili za watu hawa zimepumbaa,wameziba masikio yao,wamefumba macho yao.La sivyo, wangeona kwa macho yao,wangesikia kwa masikio yao.Wangeelewa kwa akili zao,na kunigeukia, asema Bwana,nami ningewaponya.’”

28. Halafu Paulo akasema, “Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!” [

29. Paulo alipokwisha sema hayo, Wayahudi walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao.]

30. Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu.

31. Alikuwa akihubiri ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.

Kusoma sura kamili Matendo 28