Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 27:6-15 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani.

7. Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo upepo haukuwa mwingi.

8. Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo “Bandari Nzuri,” karibu na mji wa Lasea.

9. Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo aliwapa onyo:

10. “Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu.”

11. Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo.

12. Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike. Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi.

13. Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakangoa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na pwani ya Krete.

14. Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao “Upepo wa Kaskazi” ulianza kuvuma kutoka kisiwani.

15. Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo.

Kusoma sura kamili Matendo 27