Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 27:15-30 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo.

16. Kisiwa kimoja kiitwacho Kauda kilitukinga kidogo na ule upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule mtumbwi wa meli.

17. Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libia. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli ikokotwe na upepo.

18. Dhoruba iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli.

19. Siku ya tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe.

20. Kwa muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia.

21. Baada ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema, “Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi zote.

22. Lakini sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake; meli tu ndiyo itakayopotea.

23. Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea,

24. akaniambia: ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.’

25. Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa.

26. Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani.”

27. Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huko katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu.

28. Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arubaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini.

29. Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi.

30. Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli.

Kusoma sura kamili Matendo 27