Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 26:10-24 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali.

11. Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.

12. “Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu.

13. Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu.

14. Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama ng'ombe anayepiga teke fimbo ya bwana wake.’

15. Mimi nikauliza: ‘Ni nani wewe Bwana?’ Naye Bwana akajibu: ‘Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.

16. Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonesha.

17. Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao.

18. Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.’

19. “Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hayo ya mbinguni.

20. Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao.

21. Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa hekaluni, wakajaribu kuniua.

22. Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia;

23. yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine.”

24. Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, “Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!”

Kusoma sura kamili Matendo 26