Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 23:22-35 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo.

23. Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia, “Wekeni tayari askari 200, wapandafarasi sabini na askari 200 wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku.

24. Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa.”

25. Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi:

26. “Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu!

27. “Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja na askari nikamwokoa.

28. Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa cha mashtaka yao.

29. Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu ya sehemu kadha wa kadha za sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani.

30. Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya njama za kumwua, niliamua kumleta kwako, nikawaambia washtaki wake walete mashtaka yao mbele yako.”

31. Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa; wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri.

32. Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha wale askari wapandafarasi waendelee na safari pamoja na Paulo.

33. Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na kumweka Paulo chini ya mamlaka yake.

34. Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia,

35. akasema, “Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki wako kufika.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi wa Herode.

Kusoma sura kamili Matendo 23