Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 22:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Basi, mimi nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’ Naye Bwana akaniambia, ‘Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.’

11. Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.

12. “Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko.

13. Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Saulo! Ona tena.’ Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia.

14. Halafu Anania akasema, ‘Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea.

15. Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia.

16. Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama, ubatizwe na kuondolewa dhambi zako kwa kuliungama jina lake.’

17. “Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali hekaluni, niliona maono.

18. Nilimwona Bwana akiniambia, ‘Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.’

19. Nami nikamjibu, ‘Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini.

20. Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.’

21. Naye Bwana akaniambia, ‘Nenda; nitakutuma mbali kwa mataifa mengine.’”

22. Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiliza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, “Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi.”

23. Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani.

Kusoma sura kamili Matendo 22