Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 22:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!”

2. Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema,

3. “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama nyinyi wenyewe mlivyo hivi leo.

4. Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani.

5. Kuhani mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.

6. “Basi, nilipokuwa njiani karibu na kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwanga mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote.

7. Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: ‘Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?’

8. Nami nikauliza, ‘Nani wewe, Bwana?’ Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.’

9. Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami.

10. Basi, mimi nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’ Naye Bwana akaniambia, ‘Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.’

Kusoma sura kamili Matendo 22