Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 19:26-41 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si hapa Efeso tu, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo.

27. Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha.”

28. Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!”

29. Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo.

30. Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia.

31. Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimpelekea Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo.

32. Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao.

33. Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu.

34. Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: “Mkuu ni Artemi wa Efeso!” Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili.

35. Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, “Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni.

36. Hakuna anayeweza kukana mambo hayo. Hivyo basi, tulieni; msifanye chochote bila hadhari.

37. Mmewaita watu hawa hapa ingawaje hawakuikufuru nyumba ya mungu wala kumtukana mungu wetu wa kike.

38. Kama, basi Demetrio na wafanyakazi wake wana mashtaka yao kuhusu watu hawa, yapo mahakama na wakuu wa mikoa; wanaweza kushtakiana huko.

39. Kama mna matatizo mengine, yapelekeni katika kikao halali.

40. Kwa maana tungaliweza kushtakiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na vituko vya leo. Ghasia hii haina msingi halali na hatungeweza kutoa sababu za kuridhisha za ghasia hiyo.”

41. Baada ya kusema hayo, aliuvunja mkutano.

Kusoma sura kamili Matendo 19