Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 19:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Lakini pepo mbaya aliwajibu, “Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini nyinyi ni nani?”

16. Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.

17. Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.

18. Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.

19. Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande 50,000 vya fedha.

20. Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.

21. Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, “Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia.”

22. Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia.

23. Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo njia ya Bwana.

24. Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi wake faida kubwa.

25. Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, “Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii.

26. Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si hapa Efeso tu, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo.

27. Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha.”

Kusoma sura kamili Matendo 19