Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 15:8-24 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.

9. Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.

10. Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?

11. Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tutaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.”

12. Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.

13. Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: “Ndugu zangu, nisikilizeni!

14. Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.

15. Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:

16. ‘Baada ya mambo haya nitarudi,na kujenga tena kile kibanda cha Daudi kilichoanguka;nitayatengeneza magofu yake na kukijenga tena.

17. Hapo watu wengine wote,watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu,watamtafuta Bwana.

18. Ndivyo asemavyo Bwana,aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.’

19. “Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: Tusiwataabishe watu wa mataifa wanaomgeukia Mungu.

20. Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa unajisi kwa kutambikiwa vinyago vya miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu.

21. Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato.”

22. Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu.

23. Wakawapa barua hii:“Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, tunawasalimuni nyinyi ndugu wa mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia.

24. Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu.

Kusoma sura kamili Matendo 15