Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 15:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, “Ndugu zangu, nyinyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu nitangaze Habari Njema kwa watu wa mataifa, wapate kusikia na kuamini.

8. Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.

9. Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.

10. Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?

11. Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tutaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.”

12. Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.

13. Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: “Ndugu zangu, nisikilizeni!

14. Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.

15. Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:

16. ‘Baada ya mambo haya nitarudi,na kujenga tena kile kibanda cha Daudi kilichoanguka;nitayatengeneza magofu yake na kukijenga tena.

17. Hapo watu wengine wote,watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu,watamtafuta Bwana.

18. Ndivyo asemavyo Bwana,aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.’

Kusoma sura kamili Matendo 15