Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 14:2-10 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili wawapinge hao ndugu.

3. Paulo na Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake, kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu.

4. Watu wa mji huo waligawanyika: Wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa upande wa mitume.

5. Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe.

6. Mitume walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na katika sehemu za jirani,

7. wakawa wanahubiri Habari Njema huko.

8. Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa kiwete tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe.

9. Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa,

10. akasema kwa sauti kubwa, “Simama wima kwa miguu yako!” Huyo mtu aliyelemaa miguu akainuka ghafla, akaanza kutembea.

Kusoma sura kamili Matendo 14