Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 14:15-28 Biblia Habari Njema (BHN)

15. “Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama nyinyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo.

16. Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda.

17. Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema anayowatendea: Huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake, huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha.”

18. Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu wasiwatambikie.

19. Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi nje ya mji wakidhani amekwisha kufa.

20. Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka, akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe.

21. Baada ya Paulo na Barnaba kuhubiri Habari Njema huko Derbe na kupata wafuasi wengi, walifunga safari kwenda Antiokia kwa kupitia Lustra na Ikonio.

22. Waliwaimarisha waumini wa miji hiyo na kuwatia moyo wabaki imara katika imani. Wakawaambia, “Ni lazima sisi sote kupitia katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu.”

23. Waliteua wazee katika kila kanisa kwa ajili ya waumini, kisha, kwa kusali na kufunga, wakawaweka chini ya ulinzi wa Bwana ambaye walikuwa wanamwamini.

24. Baada ya kupitia katika nchi ya Pisidia, walifika Pamfulia.

25. Baada ya kuhubiri ule ujumbe huko Perga, walikwenda Atalia.

26. Kutoka huko walisafiri kwa meli wakarudi Antiokia ambako hapo awali walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi wa neema ya Mungu kwa ajili ya kazi ambayo sasa walikuwa wameitimiza.

27. Walipofika huko Antiokia walifanya mkutano wa kanisa la mahali hapo, wakawapa taarifa juu ya mambo Mungu aliyofanya pamoja nao, na jinsi alivyowafungulia watu wa mataifa mengine mlango wa kuingia katika imani.

28. Wakakaa pamoja na wale waumini kwa muda mrefu.

Kusoma sura kamili Matendo 14