Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 13:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu.

8. Lakini huyo mchawi Elima, (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo.

9. Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi,

10. akasema, “Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka.

11. Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: Utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo.” Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze.

12. Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa mwaamini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.

13. Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane aliwaacha, akarudi Yerusalemu.

14. Lakini wao waliendelea na safari toka Perga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya sunagogi, wakakaa.

15. Baada ya masomo katika kitabu cha sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: “Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni.”

16. Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: “Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni!

17. Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua babu zetu; aliwafanya watu hawa wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu.

18. Aliwavumilia kwa muda wa miaka arubaini kule jangwani.

Kusoma sura kamili Matendo 13