Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 12:12-24 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa wamekusanyika wakisali.

13. Petro alipiga hodi kwenye mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia.

14. Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno, hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba Petro alikuwa amesimama nje mlangoni.

15. Wakamwambia yule msichana, “Una wazimu!” Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, “Huyo ni malaika wake.”

16. Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi. Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa.

17. Petro aliwaashiria kwa mkono wakae kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Kisha akawaambia watoe taarifa ya jambo hilo kwa Yakobo na wale ndugu wengine, halafu akatoka akaenda mahali pengine.

18. Kulipokucha, ulitokea wasiwasi mkubwa kati ya wale askari kuhusu yaliyokuwa yamempata Petro.

19. Herode aliamuru ufanywe msako lakini hawakuweza kumpata. Hivyo aliamuru wale askari wahojiwe, akatoa amri wauawe. Halafu akatoka huko Yudea, akaenda Kaisarea ambako alikaa.

20. Herode alikasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Lakini wao walimpelekea wajumbe. Nao wakafaulu kwanza kumpata Blasto awe upande wao. Blasto alikuwa msimamizi mkuu wa ikulu ya mfalme. Kisha, wakamwendea Herode wakamwomba kuwe na amani, kwa maana nchi yao ilitegemea nchi ya mfalme kwa chakula.

21. Siku moja iliyochaguliwa, Herode akiwa amevaa mavazi rasmi na kuketi katika kiti cha kifalme, aliwahutubia watu.

22. Wale watu walimpigia kelele za shangwe wakisema, “Hii ni sauti ya mungu, si ya mtu.”

23. Papo hapo malaika wa Bwana akamwangusha Herode chini kwa sababu hakumpa Mungu hizo sifa. Akaliwa na wadudu, akafa.

24. Neno la Mungu likazidi kuenea na kukua.

Kusoma sura kamili Matendo 12