Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 10:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kulikuwa na mtu mmoja huko Kaisarea aitwaye Kornelio, jemadari wa kikosi kimoja kiitwacho “Kikosi cha Italia.”

2. Alikuwa mtu mwema; naye pamoja na jamaa yake yote walimcha Mungu; alikuwa anafanya mengi kusaidia maskini wa Kiyahudi na alikuwa anasali daima.

3. Yapata saa tisa alasiri, aliona dhahiri katika maono malaika wa Mungu akiingia ndani na kumwambia, “Kornelio!”

4. Kornelio alimkodolea macho huyo malaika kwa hofu, akamwambia, “Kuna nini Mheshimiwa?” Huyo malaika akamwambia, “Mungu amezipokea sala na sadaka zako kwa maskini wala hatazisahau.

5. Sasa, watume watu Yopa wakamwite mtu mmoja aitwaye Simoni, kwa jina lingine Petro.

6. Yeye yumo nyumbani kwa Simoni mtengenezaji wa ngozi ambaye nyumba yake iko karibu na bahari.”

7. Huyo malaika aliyesema hayo alipokwisha kwenda zake, Kornelio aliwaita watumishi wawili wa nyumbani na mmoja wa askari zake ambaye alikuwa mcha Mungu,

8. akawaeleza yote yaliyotukia, akawatuma Yopa.

9. Kesho yake, hao watu watatu wakiwa bado safarini, lakini karibu kufika Yopa, Petro alipanda juu ya paa la nyumba yapata saa sita mchana ili kusali.

10. Aliona njaa, akatamani kupata chakula. Chakula kilipokuwa kinatayarishwa, akaota ndoto.

11. Aliona mbingu zimefunguliwa na kitu kama shuka kubwa inateremshwa chini ikiwa imeshikwa pembe zake nne.

12. Ndani ya shuka hiyo kulikuwa na kila aina ya wanyama: Wanyama wenye miguu minne, wanyama watambaao na ndege wa angani.

13. Akasikia sauti ikimwambia: “Petro, amka uchinje, ule!”

14. Petro akajibu, “La, Bwana; mimi sijaonja kamwe chochote ambacho ni najisi au kichafu.”

15. Ile sauti ikasikika tena ikimwambia: “Usiviite najisi vitu ambavyo Mungu amevitakasa!”

Kusoma sura kamili Matendo 10