Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 9:36-47 Biblia Habari Njema (BHN)

36. Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kati yao, akamkumbatia, halafu akawaambia,

37. “Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma.”

38. Yohane akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu mmoja akitoa pepo kwa kulitumia jina lako, nasi tukajaribu kumkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.”

39. Lakini Yesu akasema, “Msimkataze, maana hakuna mtu anayefanya mwujiza kwa jina langu, na papo hapo akaweza kusema mabaya juu yangu.

40. Maana, asiyepingana nasi, yuko upande wetu.

41. Mtu yeyote atakayewapeni kikombe cha maji ya kunywa, kwa sababu nyinyi ni watu wake Kristo, hakika hatakosa kupata tuzo lake.

42. “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali kwa mtu huyo kufungiwa shingoni mwake jiwe kubwa la kusagia na kutupwa baharini.

43. Mkono wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili na kwenda katika moto wa Jehanamu. [

44. Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.]

45. Na mguu wako ukikukosesha, ukate! Afadhali kuingia katika uhai bila mguu mmoja, kuliko kuwa na miguu yote miwili na kutupwa katika moto wa Jehanamu. [

46. Humo, wadudu wake hawafi na moto hauzimiki.]

47. Na jicho lako likikukosesha, lingoe! Afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja tu, kuliko kuwa na macho yako yote mawili na kutupwa katika moto wa Jehanamu.

Kusoma sura kamili Marko 9