Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 8:4-15 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Wanafunzi wake wakamwuliza, “Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?”

5. Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba.”

6. Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.

7. Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.

8. Watu wakala, wakashiba. Wakakusanya makombo wakajaza vikapu saba.

9. Nao waliokula walikuwa watu wapatao 4,000. Yesu akawaaga,

10. na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.

11. Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka afanye ishara kutoka mbinguni.

12. Yesu akahuzunika rohoni, akasema, “Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote.”

13. Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ngambo ya pili ya ziwa.

14. Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua.

15. Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.”

Kusoma sura kamili Marko 8