Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 8:15-29 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Yesu akawaonya, “Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.”

16. Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, “Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate.”

17. Yesu alitambua hayo, akawaambia, “Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu ni mizito?

18. Je, mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki

19. wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu 5,000? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki.” Wakamjibu, “Kumi na viwili.”

20. “Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu 4,000, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?” Wakamjibu, “Saba.”

21. Basi, akawaambia, “Na bado hamjaelewa?”

22. Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu, wakamwomba amguse.

23. Yesu akamshika huyo kipofu mkono, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, “Je, unaweza kuona kitu?”

24. Huyo kipofu akatazama, akasema, “Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea.”

25. Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa.

26. Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, “Usirudi kijijini!”

27. Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?”

28. Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia na wengine mmojawapo wa manabii.”

29. Naye akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.”

Kusoma sura kamili Marko 8