Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 8:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati huo, umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia,

2. “Nawaonea huruma watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa siku tatu, wala hawana chakula.

3. Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali.”

4. Wanafunzi wake wakamwuliza, “Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?”

5. Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?” Wakamjibu, “Saba.”

6. Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.

7. Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.

8. Watu wakala, wakashiba. Wakakusanya makombo wakajaza vikapu saba.

9. Nao waliokula walikuwa watu wapatao 4,000. Yesu akawaaga,

10. na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha.

11. Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka afanye ishara kutoka mbinguni.

12. Yesu akahuzunika rohoni, akasema, “Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote.”

Kusoma sura kamili Marko 8