Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 7:8-25 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Nyinyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.”

9. Yesu akaendelea kusema, “Nyinyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu!

10. Maana Mose aliamuru: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima afe’.

11. Lakini nyinyi mwafundisha, ‘Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani zawadi kwa Mungu),

12. basi, halazimiki tena kumsaidia baba yake au mama yake’.

13. Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.”

14. Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe.

15. Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu kutoka nje kinachoweza kumtia mtu unajisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu unajisi.”

16. Mwenye masikio na asikie!

17. Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano.

18. Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi,

19. kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.)

20. Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi.

21. Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,

22. uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.

23. Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.”

24. Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha.

25. Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.

Kusoma sura kamili Marko 7