Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 7:18-36 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Naye akawaambia, “Je, hata nyinyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu kutoka nje, hakiwezi kumtia unajisi,

19. kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alihalalisha vyakula vyote.)

20. Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia unajisi.

21. Maana kutoka ndani, moyoni mwa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,

22. uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.

23. Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu unajisi.”

24. Yesu aliondoka hapo, akaenda wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha.

25. Hapo mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.

26. Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu.

27. Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

28. Lakini huyo mama akasema, “Ni kweli, Bwana; lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.”

29. Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!”

30. Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.

31. Kisha Yesu aliondoka wilaya ya Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli.

32. Basi, wakamletea bubu kiziwi, wakamwomba amwekee mikono.

33. Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi.

34. Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake “Funguka.”

35. Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa.

36. Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo.

Kusoma sura kamili Marko 7