Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 6:6-19 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Alishangaa sana kwa sababu ya kutoamini kwao.Kisha Yesu alivitembelea vijiji vya pale karibu akiwafundisha watu.

7. Aliwaita wale wanafunzi kumi na wawili, akaanza kuwatuma wawiliwawili. Aliwapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu;

8. akawaamuru: “Msichukue chochote mnapokwenda isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kibindoni.

9. Vaeni viatu lakini msichukue koti la ziada.”

10. Tena aliwaambia, “Popote mtakapokaribishwa nyumbani, kaeni humo mpaka mtakapoondoka mahali hapo.

11. Mahali popote ambapo watu watakataa kuwakaribisheni au kuwasikiliza, ondokeni hapo na kuyakunguta mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao.”

12. Basi, wakaondoka, wakahubiri watu watubu.

13. Waliwafukuza pepo wengi wabaya; wakawapaka mafuta wagonjwa wengi, wakawaponya.

14. Basi, mfalme Herode alisikia juu ya hayo yote, maana sifa za Yesu zilienea kila mahali. Baadhi ya watu walikuwa wakisema, “Yohane Mbatizaji amefufuka kutoka kwa wafu, ndiyo maana nguvu hizi zinafanya kazi ndani yake.”

15. Wengine walisema, “Mtu huyu ni Elia.” Wengine walisema, “Huyu ni nabii kama mmojawapo wa manabii wa kale.”

16. Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, “Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.”

17. Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake.

18. Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako.”

19. Basi, Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumuua, asiweze.

Kusoma sura kamili Marko 6