Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 6:38-49 Biblia Habari Njema (BHN)

38. Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni kutazama.” Walipokwisha tazama, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39. Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi.

40. Nao wakaketi makundimakundi ya watu 100 na ya watu hamsini.

41. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote.

42. Watu wote wakala, wakashiba.

43. Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili.

44. Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume 5,000.

45. Mara Yesu akawaamuru wanafunzi wake wapande mashua, wamtangulie kwenda Bethsaida, ngambo ya ziwa, wakati yeye anauaga umati wa watu.

46. Baada ya kuwaaga watu alikwenda mlimani kusali.

47. Ilipokuwa jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, naye alikuwa peke yake katika nchi kavu.

48. Basi, akawaona wanafunzi wake wakitaabika kwa kupiga makasia, maana upepo ulikuwa unawapinga. Karibu na mapambazuko, Yesu aliwaendea wanafunzi akitembea juu ya maji, akataka kuwapita.

49. Lakini walipomwona akitembea juu ya maji, walidhani ni mzimu, wakapiga yowe.

Kusoma sura kamili Marko 6