Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 6:16-30 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Lakini Herode alipopata habari hizi alisema, “Huyu ni Yohane! Nilimkata kichwa, lakini amefufuka.”

17. Hapo awali Herode mwenyewe alikuwa ameamuru Yohane atiwe nguvuni, akamfunga gerezani. Herode alifanya hivyo kwa sababu ya Herodia ambaye Herode alimwoa ingawaje alikuwa mke wa Filipo, ndugu yake.

18. Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kumchukua mke wa ndugu yako.”

19. Basi, Herodia alimchukia sana Yohane, akataka kumuua, asiweze.

20. Herode alimwogopa Yohane kwa maana alijua kwamba yeye ni mtu mwema na mtakatifu, na hivyo akamlinda. Herode alipenda kumsikiliza Yohane, ingawaje baada ya kumsikiliza, alifadhaika sana.

21. Ndipo ikapatikana nafasi, wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode. Herode aliwafanyia karamu wazee wa baraza lake, majemadari na viongozi wa Galilaya.

22. Basi, binti yake Herodia aliingia, akacheza, akawafurahisha sana Herode na wageni wake. Mfalme akamwambia huyo msichana, “Niombe chochote utakacho, nami nitakupa.”

23. Tena akamwapia, “Chochote utakachoniomba, nitakupa; hata ikiwa ni nusu ya ufalme wangu.”

24. Hapo huyo msichana akatoka, akamwuliza mama yake, “Niombe nini?” Naye akamjibu, “Kichwa cha Yohane Mbatizaji.”

25. Msichana akamrudia mfalme mbio akamwomba, “Nataka unipe sasa hivi katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.”

26. Mfalme akahuzunika sana, lakini kwa sababu ya kiapo chake, na kwa ajili ya wale wageni wake karamuni, hakutaka kumkatalia.

27. Basi, mfalme akamwamuru askari kukileta kichwa cha Yohane. Askari akaenda, akamkata kichwa Yohane mle gerezani,

28. akakileta katika sinia, akampa msichana naye msichana akampa mama yake.

29. Wanafunzi wa Yohane walipopata habari, walikwenda wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

30. Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha.

Kusoma sura kamili Marko 6