Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 4:24-34 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Akawaambia pia, “Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa.

25. Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.”

26. Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani.

27. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika.

28. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke.

29. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.”

30. Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani?

31. Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote.

32. Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.”

33. Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia.

34. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.

Kusoma sura kamili Marko 4