Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 14:19-34 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Hapo wanafunzi wake wakaanza kuhuzunika, wakamwuliza mmojammoja, “Je, ni mimi?”

20. Yesu akawaambia, “Ni mmoja wenu nyinyi kumi na wawili, anayechovya mkate pamoja nami katika bakuli.

21. Kweli Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yanavyosema juu yake; lakini, ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa!”

22. Walipokuwa wanakula, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na kuwapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni; huu ni mwili wangu.”

23. Kisha akatwaa kikombe cha divai, akamshukuru Mungu, akawapa; wote wakanywa kutoka kikombe hicho.

24. Akawaambia, “Hii ni damu yangu inayothibitisha agano la Mungu, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi.

25. Kweli nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa upya katika ufalme wa Mungu.”

26. Kisha wakaimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.

27. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Nyinyi nyote mtakuwa na mashaka nami; maana Maandiko Matakatifu yasema:‘Nitampiga mchungaji,nao kondoo watatawanyika.’

28. Lakini nikisha fufuka, nitawatangulieni kule Galilaya.”

29. Petro akamwambia “Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakukana kamwe!”

30. Yesu akamwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.”

31. Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakuacha kamwe.” Wanafunzi wote pia wakasema vivyo hivyo.

32. Basi, wakafika katika bustani iliyoitwa Gethsemane. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati mimi nasali.”

33. Kisha akawachukua Petro, Yakobo na Yohane; akaanza kufadhaika sana na kuhangaika.

34. Akawaambia, “Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa na kukesha.”

Kusoma sura kamili Marko 14