Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 13:21-37 Biblia Habari Njema (BHN)

21. “Basi mtu akiwaambieni, ‘Tazama, Kristo yupo hapa,’ au ‘Yupo pale,’ msimsadiki.

22. Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, kwa ajili ya kuwapotosha wateule wa Mungu kama ikiwezekana.

23. Lakini nyinyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.

24. “Basi, siku hizo, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza.

25. Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.

26. Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu.

27. Kisha atawatuma malaika wake wawakusanye wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.

28. “Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa mavuno umekaribia.

29. Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.

30. Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.

31. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

32. “Lakini, juu ya siku au saa hiyo hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.

33. Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini.

34. Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia na mlinzi wa mlango awe macho.

35. Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.

36. Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.

37. Ninayowaambieni nyinyi, nawaambia wote: Kesheni!”

Kusoma sura kamili Marko 13