Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 11:18-33 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Makuhani wakuu na waalimu wa sheria waliposikia hayo, walianza kutafuta njia ya kumwangamiza. Lakini walimwogopa kwa sababu umati wa watu ulishangazwa na mafundisho yake.

19. Ilipokuwa jioni, Yesu na wanafunzi wake waliondoka mjini.

20. Asubuhi na mapema, walipokuwa wanapita, waliuona ule mtini umenyauka wote, hata mizizi.

21. Petro aliukumbuka, akamwambia Yesu, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani, umenyauka!”

22. Yesu akawaambia, “Mwaminini Mungu.

23. Nawaambieni kweli, mtu akiuambia mlima huu: ‘Ngoka ukajitose baharini,’ bila kuona shaka moyoni mwake, ila akaamini kwamba mambo yote anayosema yanafanyika, atafanyiwa jambo hilo.

24. Kwa hiyo nawaambieni, mnaposali na kuomba kitu, aminini kwamba mmekipokea, nanyi mtapewa.

25. Mnaposimama kusali, msameheni kila mtu aliyewakosea chochote, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe nyinyi makosa yenu.” [

26. Lakini msipowasamehe wengine, hata Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe nyinyi makosa yenu.]

27. Basi, wakafika tena Yerusalemu. Yesu alipokuwa akitembea hekaluni, makuhani wakuu, waalimu wa sheria na wazee walimwendea,

28. wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani aliyekupa mamlaka ya kufanya mambo haya?”

29. Lakini Yesu akawaambia, “Nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, nami pia nitawaambia ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.

30. Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka mbinguni ama kwa watu? Nijibuni.”

31. Wakaanza kujadiliana, “Tukisema, ‘Yalitoka mbinguni’, atatuuliza, ‘Basi, mbona hamkumsadiki?’

32. Na tukisema, ‘Yalitoka kwa watu (Waliogopa umati wa watu maana wote waliamini kwamba Yohane alikuwa kweli nabii.)

33. Basi, wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.”

Kusoma sura kamili Marko 11