Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 10:42-52 Biblia Habari Njema (BHN)

42. Hivyo, Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba wale wanaofikiriwa kuwa watawala wa mataifa huwatawala watu wao kwa mabavu, na wakuu hao huwamiliki watu wao.

43. Lakini kwenu isiwe hivyo, ila anayetaka kuwa mkubwa kati yenu, sharti awe mtumishi wenu.

44. Anayetaka kuwa wa kwanza, sharti awe mtumishi wa wote.

45. Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, ila kutumikia, na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”

46. Basi, wakafika Yeriko, naye Yesu alipokuwa anatoka katika mji huo akiwa na wanafunzi wake pamoja na umati mkubwa wa watu, kipofu, mwana wa Timayo aitwaye Bartimayo, alikuwa ameketi kando ya barabara, anaomba maskini.

47. Aliposikia kwamba ni Yesu wa Nazareti aliyekuwa anapita mahali hapo, alianza kupaza sauti, “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!”

48. Watu wengi walimkemea ili anyamaze, lakini yeye akazidi kupaza sauti, “Mwana wa Daudi, nihurumie!”

49. Yesu alisimama, akasema, “Mwiteni.” Basi, wakamwita huyo kipofu, wakamwambia, “Jipe moyo! Simama, anakuita.”

50. Naye akatupilia mbali vazi lake, akaruka juu, akamwendea Yesu.

51. Yesu akamwuliza, “Unataka nikufanyie nini?” Huyo kipofu akamwambia, “Mwalimu, naomba nipate kuona.”

52. Yesu akamwambia, “Nenda, imani yako imekuponya.” Mara huyo kipofu akaweza kuona, akamfuata Yesu njiani.

Kusoma sura kamili Marko 10