Agano la Kale

Agano Jipya

Marko 1:31-45 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.

32. Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo.

33. Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.

34. Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.

35. Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali.

36. Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta.

37. Walipomwona, wakamwambia, “Kila mtu anakutafuta.”

38. Yesu akawaambia, “Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo.”

39. Basi, akaenda kila mahali huko Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.

40. Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba: “Ukitaka, waweza kunitakasa!”

41. Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, “Nataka! Takasika!”

42. Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika.

43. Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwambia,

44. “Angalia usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani na ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”

45. Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

Kusoma sura kamili Marko 1