Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 9:25-37 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe?

26. Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.

27. Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.”

28. Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali.

29. Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kungaa sana.

30. Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao walikuwa Mose na Elia,

31. ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kutoka kwake ambako angekamilisha huko Yerusalemu.

32. Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.

33. Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Basi, tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Kwa kweli hakujua anasema nini.

34. Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana.

35. Sauti ikasikika kutoka katika hilo wingu: “Huyu ndiye Mwanangu niliyemchagua, msikilizeni.”

36. Baada ya hiyo sauti kusikika, Yesu alionekana akiwa peke yake. Wanafunzi walikaa kimya juu ya tukio hilo, na wakati ule hawakumwambia mtu yeyote mambo hayo waliyoyaona.

37. Kesho yake walipokuwa wakishuka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu.

Kusoma sura kamili Luka 9