Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 9:19-34 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Nao wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa wewe ni Yohane Mbatizaji; wengine, Elia; wengine, mmojawapo wa manabii wa kale ambaye amefufuka.”

20. Hapo akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo wa Mungu.”

21. Halafu Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hiyo.

22. Akaendelea kusema kwamba ni lazima Mwana wa Mtu apate mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na waalimu wa sheria na kuuawa, lakini siku ya tatu atafufuliwa.

23. Kisha akawaambia watu wote, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate.

24. Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa.

25. Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe?

26. Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu.

27. Nawaambieni kweli, kuna wengine papa hapa ambao hawatakufa kabla ya kuuona ufalme wa Mungu.”

28. Yapata siku nane baada ya kusema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali.

29. Alipokuwa akisali, sura yake ilibadilika, mavazi yake yakawa meupe na kungaa sana.

30. Na watu wawili wakaonekana wakizungumza naye, nao walikuwa Mose na Elia,

31. ambao walitokea wakiwa wenye utukufu, wakazungumza naye juu ya kutoka kwake ambako angekamilisha huko Yerusalemu.

32. Petro na wenzake walikuwa wamelemewa na usingizi mzito, hata hivyo waliamka, wakauona utukufu wake, wakawaona na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.

33. Basi, watu hao wawili walipokuwa wakiondoka, Petro alimwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa! Basi, tujenge vibanda vitatu: Kimoja chako, kimoja cha Mose na kimoja cha Elia.” Kwa kweli hakujua anasema nini.

34. Petro alipokuwa akisema hayo, mara wingu likatokea na kuwafunika; na wingu hilo lilipowajia, wale wanafunzi waliogopa sana.

Kusoma sura kamili Luka 9