Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 8:41-56 Biblia Habari Njema (BHN)

41. Hapo akaja mtu mmoja aitwaye Yairo, ofisa wa sunagogi. Alijitupa miguuni pa Yesu, akamwomba aende nyumbani kwake,

42. kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.Yesu alipokuwa akienda, watu wakawa wanamsonga kila upande.

43. Basi, kulikuwa na mwanamke mmoja kati ya lile kundi la watu, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili; ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote kwa waganga, hakuna aliyefaulu kumponya.

44. Huyo mwanamke alimfuata Yesu nyuma, akagusa pindo la vazi lake. Papo hapo akaponywa ugonjwa wake wa kutokwa damu.

45. Yesu akasema, “Ni nani aliyenigusa?” Wote wakasema kwamba hapakuwa na mtu aliyemgusa. Naye Petro akasema, “Bwana, umati wa watu umekuzunguka na kukusonga!”

46. Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, maana nimehisi nguvu imenitoka.”

47. Yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kujificha, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa mbele ya Yesu. Hapo akaeleza mbele ya wote kisa cha kumgusa Yesu na jinsi alivyoponywa mara moja.

48. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda na amani.”

49. Alipokuwa bado akiongea, Yairo akaletewa habari kutoka nyumbani: “Binti yako amekwisha kufa, ya nini kumsumbua Mwalimu zaidi?”

50. Yesu aliposikia hayo akamwambia Yairo, “Usiogope; amini tu, naye atapona.”

51. Alipofika nyumbani hakumruhusu mtu kuingia ndani pamoja naye, isipokuwa Petro, Yohane, Yakobo na wazazi wa huyo msichana.

52. Watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili yake. Lakini Yesu akawaambia, “Msilie, kwa maana mtoto hajafa, amelala tu!”

53. Nao wakamcheka kwa sababu walijua kwamba alikuwa amekufa.

54. Lakini Yesu akamshika mkono akasema, “Mtoto, amka!”

55. Roho yake ikamrudia, akaamka mara. Yesu akaamuru wampe chakula.

56. Wazazi wake walishangaa, lakini Yesu akawaamuru wasimwambie mtu yeyote hayo yaliyotendeka.

Kusoma sura kamili Luka 8