Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 7:36-50 Biblia Habari Njema (BHN)

36. Mfarisayo mmoja alimwalika Yesu kula chakula nyumbani kwake. Akaingia nyumbani kwa huyo Mfarisayo, akakaa kula chakula.

37. Basi, katika mji ule kulikuwa na mama mmoja mwenye dhambi. Alipopata habari kwamba Yesu yuko nyumbani kwa huyo Mfarisayo, alichukua chupa ya alabasta yenye marashi.

38. Akaja, akasimama karibu na miguu yake Yesu, akilia, na machozi yake yakamdondokea Yesu miguuni. Huyo mwanamke akaipangusa miguu ya Yesu kwa nywele zake. Kisha akaibusu na kuipaka yale marashi.

39. Yule Mfarisayo aliyemwalika Yesu alipoona hayo, akawaza moyoni mwake, “Kama mtu huyu angekuwa kweli nabii angejua huyu mwanamke ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.”

40. Yesu akamwambia huyo Mfarisayo, “Simoni, ninacho kitu cha kukuambia.” Naye Simoni akamwambia, “Ndio Mwalimu, sema.” Yesu akasema,

41. “Watu wawili walikuwa wamemkopa mtu fedha: Mmoja alikuwa amekopa denari 500, na mwingine hamsini.

42. Waliposhindwa kulipa madeni yao, huyo mtu aliwasamehe wote wawili. Sasa ni yupi kati ya hao wawili atampenda zaidi huyo bwana?”

43. Simoni akamjibu, “Ni dhahiri kwamba yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi atampenda zaidi yule bwana.” Yesu akamwambia, “Sawa.”

44. Halafu akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona huyu mwanamke, sivyo? Basi, mimi nilipoingia hapa nyumbani kwako hukunipa maji ya kunawa miguu yangu; lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kunipangusa kwa nywele zake.

45. Wewe hukunisalimu kwa kunibusu, lakini huyu mwanamke tangu nilipoingia hapa amekuwa akiibusu miguu yangu.

46. Wewe hukunionesha ukarimu wako kwa kunipaka mafuta kichwani, lakini huyu mwanamke amefanya hivyo kwa kunipaka mafuta miguu yangu.

47. Kwa hiyo nakuambia amesamehewa dhambi zake nyingi kwa kuwa ameonesha upendo mkubwa. Mwenye kusamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

48. Basi, Yesu akamwambia yule mwanamke, “Umesamehewa dhambi zako.”

49. Ndipo wale waliokuwa pamoja naye mezani wakaulizana, “Ni mtu wa namna gani huyu awezaye kusamehe dhambi?”

50. Naye Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

Kusoma sura kamili Luka 7