Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 6:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka, simama katikati.” Yule mtu akaenda kusimama katikati.

9. Kisha Yesu akawaambia, “Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

10. Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena.

11. Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.

12. Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akisali.

13. Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akawachagua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume:

14. Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo,

15. Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote),

16. Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.

17. Baada ya kushuka mlimani pamoja nao, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo kulikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao.

18. Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu.

19. Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.

20. Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema:“Heri nyinyi mlio maskini,maana ufalme wa Mungu ni wenu.

21. Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa,maana baadaye mtashiba.Heri nyinyi mnaolia sasa,maana baadaye mtacheka kwa furaha.

Kusoma sura kamili Luka 6