Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 6:31-39 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.

32. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.

33. Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo.

34. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile.

35. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya.

36. Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.

37. “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa.

38. Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”

39. Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni.

Kusoma sura kamili Luka 6