Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 6:24-38 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri,maana mmekwisha pata faraja yenu.

25. Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa,maana baadaye mtasikia njaa.Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa,maana baadaye mtaomboleza na kulia.

26. Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu,maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.

27. “Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni.

28. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya.

29. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako.

30. Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie.

31. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo.

32. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.

33. Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo.

34. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile.

35. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya.

36. Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma.

37. “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa.

38. Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.”

Kusoma sura kamili Luka 6