Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 5:7-25 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama.

8. Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, “Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!”

9. Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile.

10. Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu.”

11. Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.

12. Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”

13. Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika!” Mara ule ukoma ukamwacha.

14. Naye Yesu akamwamuru: “Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose kuwathibitishia kwamba umepona.”

15. Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.

16. Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.

17. Siku moja, Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na waalimu wa sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponya wagonjwa.

18. Mara watu wakaja, wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani, wamweke mbele ya Yesu.

19. Lakini, kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya paa, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu.

20. Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.”

21. Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!”

22. Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu?

23. Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’

24. Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.”

25. Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu.

Kusoma sura kamili Luka 5