Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 5:15-29 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.

16. Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.

17. Siku moja, Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na waalimu wa sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponya wagonjwa.

18. Mara watu wakaja, wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani, wamweke mbele ya Yesu.

19. Lakini, kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya paa, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu.

20. Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, “Rafiki, umesamehewa dhambi zako.”

21. Waalimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: “Nani huyu anayesema maneno ya kufuru? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!”

22. Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, “Mnawaza nini mioyoni mwenu?

23. Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi,’ au kusema, ‘Simama utembee?’

24. Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kuwasamehe watu dhambi duniani.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Simama, chukua kitanda chako, uende zako nyumbani.”

25. Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda nyumbani kwake huku akimtukuza Mungu.

26. Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: “Tumeona maajabu leo.”

27. Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtozaushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, “Nifuate!”

28. Naye akaacha yote akamfuata.

29. Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake. Na kundi kubwa la watozaushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao.

Kusoma sura kamili Luka 5