Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 4:32-44 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.

33. Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:

34. “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”

35. Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.

36. Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”

37. Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile.

38. Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.

39. Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia.

40. Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.

41. Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walijua kwamba yeye ndiye Kristo.

42. Kesho yake asubuhi, Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta. Hao watu walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.

43. Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.”

44. Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.

Kusoma sura kamili Luka 4