Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 4:23-36 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: ‘Mganga jiponye mwenyewe,’ na pia mtasema: ‘Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye pia hapa kijijini mwako.’”

24. Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi kijijini mwake.

25. Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Elia. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.

26. Hata hivyo, Elia hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarefathi katika Sidoni.

27. Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani mwenyeji wa Siria.”

28. Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.

29. Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.

30. Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.

31. Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu wilayani Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.

32. Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.

33. Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:

34. “Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”

35. Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.

36. Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”

Kusoma sura kamili Luka 4