Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 24:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Hapo hao wanawake wakayakumbuka maneno yake,

9. wakarudi kutoka kaburini, wakawapa mitume wale kumi na mmoja na wafuasi wengine habari za mambo hayo yote.

10. Hao waliotoa habari hizo kwa mitume ni: Maria Magdalene, Yoana na Maria mama wa Yakobo, pamoja na wanawake wengine walioandamana nao.

11. Mitume waliyachukua maneno hayo kama yasiyo na msingi, hivyo hawakuamini.

12. Lakini Petro alitoka, akaenda mbio hadi kaburini. Alipoinama kuchungulia ndani, akaiona tu ile sanda. Akarudi nyumbani huku akiwa anashangaa juu ya hayo yaliyotokea.

13. Siku hiyohiyo, wawili kati ya wafuasi wake Yesu wakawa wanakwenda katika kijiji kimoja kiitwacho Emau, umbali wa kilomita kumi na moja kutoka Yerusalemu.

14. Wakawa wanazungumza juu ya hayo yote yaliyotukia.

15. Walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akatokea, akatembea pamoja nao.

16. Walimwona kwa macho, lakini hawakumtambua.

17. Akawauliza, “Mnazungumza nini huku mnatembea?” Nao wakasimama kimya, nyuso zao wamezikunja kwa huzuni.

18. Mmoja, aitwaye Kleopa, akamjibu, “Je, wewe ni mgeni peke yako Yerusalemu ambaye hujui yaliyotukia huko siku hizi?”

19. Naye akawajibu, “Mambo gani?” Wao wakamjibu, “Mambo yaliyompata Yesu wa Nazareti. Yeye alikuwa nabii mwenye uwezo wa kutenda na kufundisha mbele ya Mungu na mbele ya watu wote.

20. Makuhani na watawala wetu walimtoa ahukumiwe kufa, wakamsulubisha.

21. Lakini sisi tulitumaini kwamba yeye ndiye angeikomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu mambo hayo yalipotendeka.

Kusoma sura kamili Luka 24