Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 22:52-61 Biblia Habari Njema (BHN)

52. Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa hekalu na wazee waliokuja kumkamata: “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi?

53. Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza.”

54. Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali.

55. Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja, naye Petro akiwa miongoni mwao.

56. Mtumishi mmoja wa kike alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, “Mtu huyu pia alikuwa pamoja na Yesu.”

57. Lakini Petro akakana akisema, “Wee! Simjui mimi.”

58. Baadaye kidogo, mtu mwingine akamwona Petro, akasema, “Wewe ni mmoja wao.” Lakini Petro akajibu “Bwana wee; si mimi!”

59. Kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasisitiza, “Hakika huyu alikuwa pamoja naye; ametoka Galilaya ati.”

60. Lakini Petro akasema, “Bwana wee; sijui hata unachosema!” Na papo hapo, akiwa bado anaongea, jogoo akawika.

61. Bwana akageuka na kumtazama Petro, naye Petro akakumbuka yale aliyokuwa ameambiwa na Bwana: “Leo kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

Kusoma sura kamili Luka 22