Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 22:45-57 Biblia Habari Njema (BHN)

45. Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni.

46. Akawaambia, “Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi.”

47. Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu.

48. Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?”

49. Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, “Bwana, tutumie panga zetu?”

50. Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio lake la kulia.

51. Hapo, Yesu akasema, “Acha! Hii inatosha.” Akaligusa sikio la mtu huyo, akaliponya.

52. Kisha Yesu akawaambia makuhani wakuu, wakubwa wa walinzi wa hekalu na wazee waliokuja kumkamata: “Je, mmekuja na mapanga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyanganyi?

53. Nilipokuwa pamoja nanyi kila siku hekaluni hamkunitia nguvuni. Lakini, huu ndio wakati wenu hasa, ndio wakati wa utawala wa giza.”

54. Basi, wakamkamata, wakamchukua na kwenda naye nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro akawa anamfuata nyuma kwa mbali.

55. Moto ulikuwa umewashwa katikati ya ua, nao wakawa wameketi pamoja, naye Petro akiwa miongoni mwao.

56. Mtumishi mmoja wa kike alipomwona Petro ameketi karibu na moto, akamkodolea macho, akasema, “Mtu huyu pia alikuwa pamoja na Yesu.”

57. Lakini Petro akakana akisema, “Wee! Simjui mimi.”

Kusoma sura kamili Luka 22