Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 22:36-51 Biblia Habari Njema (BHN)

36. Naye akawaambia, “Lakini sasa, yule aliye na mfuko wa fedha auchukue; na aliye na mkoba, hali kadhalika. Na yeyote asiye na upanga, auze koti lake anunue mmoja.

37. Maana nawaambieni, haya maneno ya Maandiko Matakatifu: ‘Aliwekwa kundi moja na wahalifu,’ ni lazima yatimie. Naam, yale yanayonihusu yanafikia ukamilifu wake.”

38. Nao wakasema, “Bwana, tazama; hapa kuna panga mbili.” Naye akasema, “Basi!”

39. Yesu akatoka, na kama ilivyokuwa desturi yake, akaenda katika mlima wa Mizeituni; wanafunzi wake wakamfuata.

40. Alipofika huko akawaambia, “Salini, msije mkaingia katika kishawishi.”

41. Kisha akawaacha, akaenda umbali wa mtu kuweza kutupa jiwe, akapiga magoti, akasali:

42. “Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki; hata hivyo, mapenzi yako yatimizwe, wala siyo yangu.”

43. Hapo, malaika kutoka mbinguni akamtokea ili kumtia moyo.

44. Akiwa katika uchungu mkubwa, alisali kwa bidii zaidi; na jasho likamtoka kama matone ya damu, likatiririka mpaka chini.

45. Baada ya kusali, aliwarudia wanafunzi wake, akawakuta wamelala, kwani walikuwa na huzuni.

46. Akawaambia, “Mbona mnalala? Amkeni msali, msije mkaingia katika kishawishi.”

47. Alipokuwa bado anaongea, kundi la watu likaja likiongozwa na yule aliyeitwa Yuda, mmoja wa wale mitume kumi na wawili. Yuda akaenda kumsalimu Yesu kwa kumbusu.

48. Lakini Yesu akamwambia, “Yuda! Je, unamsaliti Mwana wa Mtu kwa kumbusu?”

49. Wale wanafunzi wake walipoona hayo wakasema, “Bwana, tutumie panga zetu?”

50. Na mmoja wao akampiga upanga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio lake la kulia.

51. Hapo, Yesu akasema, “Acha! Hii inatosha.” Akaligusa sikio la mtu huyo, akaliponya.

Kusoma sura kamili Luka 22