Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 21:23-35 Biblia Habari Njema (BHN)

23. Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa.

24. Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.

25. “Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.

26. Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.

27. Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.

28. Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.”

29. Kisha akawaambia mfano: “Angalieni mtini na miti mingine yote.

30. Mnapoona kwamba imeanza kuchipua majani, mwatambua kwamba majira ya mavuno yamekaribia.

31. Vivyo hivyo, mtakapoona mambo hayo yanatendeka, mtatambua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.

32. Kweli nawaambieni, kizazi hiki cha sasa hakitapita kabla ya hayo yote kutendeka.

33. Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

34. “Muwe macho, mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na shughuli za maisha haya. La sivyo, siku ile itawajieni ghafla.

35. Kwa maana itawajia kama mtego wote wanaoishi duniani pote.

Kusoma sura kamili Luka 21