Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 21:11-28 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kila mahali kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, njaa na tauni. Kutakuwa na vituko vya kutisha na ishara kubwa angani.

12. Lakini kabla ya kutokea hayo yote, watawatieni nguvuni, watawatesa na kuwapelekeni katika masunagogi na kuwatia gerezani; mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya jina langu,

13. mpate kunishuhudia kwao.

14. Muwe na msimamo huu mioyoni mwenu: Hakuna kufikiria kabla ya wakati juu ya jinsi mtakavyojitetea,

15. kwa sababu mimi mwenyewe nitawapeni ufasaha wa maneno na hekima, hata maadui zenu hawataweza kustahimili wala kupinga.

16. Wazazi wenu, ndugu, jamaa na rafiki zenu watawasaliti nyinyi; na baadhi yenu mtauawa.

17. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu.

18. Lakini, hata unywele mmoja wa vichwa vyenu hautapotea.

19. Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu.

20. “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi jueni ya kwamba wakati umefika ambapo mji huo utaharibiwa.

21. Hapo, walioko Yudea wakimbilie milimani; wale walio mjini watoke; na wale walio mashambani wasirudi mjini.

22. Kwa maana siku hizo ni siku za adhabu, ili yote yaliyoandikwa yatimie.

23. Ole wao waja wazito na wanyonyeshao siku hizo! Kwa maana kutakuwa na dhiki kubwa katika nchi, na hasira ya Mungu itawajia watu hawa.

24. Wengine watauawa kwa upanga, wengine watachukuliwa mateka katika nchi zote; na mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa mataifa mengine, hadi nyakati zao zitakapotimia.

25. “Kutakuwa na ishara katika jua na mwezi na nyota. Mataifa duniani yatakuwa na dhiki kwa sababu ya wasiwasi kutokana na mshindo wa mawimbi ya bahari.

26. Watu watazirai kwa sababu ya woga, wakitazamia mambo yatakayoupata ulimwengu; kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.

27. Halafu, watamwona Mwana wa Mtu akija katika wingu, mwenye nguvu na utukufu mwingi.

28. Wakati mambo hayo yatakapoanza kutukia, simameni na kuinua vichwa vyenu juu, kwa maana ukombozi wenu umekaribia.”

Kusoma sura kamili Luka 21