Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 20:15-27 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Basi, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamuua.” Yesu akauliza, “Yule mwenye shamba atawafanya nini hao wakulima?

16. Atakuja kuwaangamiza wakulima hao, na kuwapa wakulima wengine hilo shamba la mizabibu.” Watu waliposikia maneno hayo, walisema: “Hasha! Yasitukie hata kidogo!”

17. Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Maandiko haya Matakatifu yana maana gani, basi?‘Jiwe walilokataa waashi,sasa limekuwa jiwe kuu la msingi!’

18. Mtu yeyote akianguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda.”

19. Waalimu wa sheria na makuhani wakuu walifahamu kwamba mfano huo ulikuwa unawahusu, na hivyo walitaka kumkamata palepale, ila tu waliogopa watu.

20. Basi, wakawa wanatafuta wakati wa kufaa. Wakawahonga watu fulani wajisingizie kuwa wema, wakawatuma wamnase Yesu kwa maswali, na hivyo waweze kumtia nguvuni na kumpeleka kwa wakuu wa serikali.

21. Hao wapelelezi wakamwambia, “Mwalimu, tunajua kwamba unasema na kufundisha mambo ya kweli; tunajua kwamba wewe huna ubaguzi; wewe wafundisha ukweli juu ya njia ya Mungu.

22. Basi, tuambie kama ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari!”

23. Yesu alitambua mtego wao, akawaambia,

24. “Nionesheni sarafu. Je, sura na chapa ni vya nani?”

25. Nao wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.”

26. Hawakufaulu kumnasa kwa neno lolote pale mbele ya watu na hivyo wakakaa kimya wakilistaajabia jibu lake.

27. Kisha Masadukayo, ambao husema kwamba wafu hawafufuki, wakamjia Yesu, wakasema:

Kusoma sura kamili Luka 20